KIPA SPURS AWAGOMEA MANCHESTER UNITED.

12/29/2014 03:55:00 pm
KIPA wa Tottenham Hotspur, Hugo Lloris, amekuwa nyota wa mchezo baada ya kucheza kwa kiwango kikubwa kuwagomea washambuliaji wa Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliomalizika kwa sare ya bila kufungana jana Jumapili.
Kipa huyo aliokoa hatari kadhaa zilizokaribia kuwa mabao baada ya washambuliaji wa Man United kuonyesha uchu katika kipindi cha kwanza kabla ya umahiri wa golikipa huyo kuifanya timu yake kuambulia pointi kutokana na sare hiyo uwanjani White Hart Lane.
Man United, ambayo imeshinda mechi saba kati ya nane za karibuni, inaendelea kubaki kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo wakati Spurs ikiwa nafasi ya sita, lakini ikisubiri matokeo ya Arsenal na West Ham United ambazo pia zilitarajia kumenyana baadaye jana.
Man United iligongesha mwamba kabla ya mpira wa kichwa ulionekana kuvuka mstari wa goli kukataliwa kuwa bao kwa madai kwamba Phil Jones alikuwa ameotea. Spurs nao walipoteza nafasi yao ya kufunga kupitia kwa Ryan Mason, aliyepaisha mpira katika dakika za mwishoni.
Chelsea nayo ilijikuta katika hali kama hiyo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Southampton. Southampton ilipata bao lake dakika ya 17 kupitia Mane, bao la Chelsea lilifungwa na Eden Hazard dakika ya 44.

0 comments:

Post a Comment