OLD TRAFORD YAWA SALAMA MIKONONI MWA DAVID DE GEA:

12/21/2014 12:42:00 pm
LANGO la Manchester United liko salama kuliko wakati mwingine wowote tangu kuondoka kwa Edwin van Der Sar mwaka 2011. Kipa David de Gea ameliweka lango hilo katika mikono salama kabisa kama inavyozidi kujidhihirisha katika miaka ya karibuni.

Akulia Madrid, Waingereza wamnyatia

De Gea alizaliwa Madrid ambao ni Mji Mkuu wa Hispania, mnamo Novemba 7, 1990. Alijiunga na Atletico Madrid akiwa na umri wa miaka 13 baada ya kocha wake katika timu ya mtaani, Juan Luis Martin kuidanganya timu hiyo kuwa klabu ya Rayo Vallecano ilikuwa inataka kumchukua.

Alitesa katika soka la vijana mpaka klabu hiyo ilipompatia mkataba wa kulipwa mwaka 2008 akiwa na umri wa miaka 17. Mkataba huo ulikuwa unamuweka Atletico mpaka mwaka 2011.

Akiwa bado katika timu ya vijana, mnamo mwaka 2009 katika dirisha la majira ya joto klabu ya QPR ya England ilianza kumfukuzia kwa uhamuisho wa mkopo.

De Gea alikataa uhamisho huo hali iliyoilazimisha klabu hiyo kumuadhibu kwa kumtaka afanye mazoezi peke yake. Wiki kadhaa baadaye, kocha wa Atletico wakati huo, Abel Resino aligundua kuwa De Gea alikuwa anafanya mazoezi peke yake katika timu ya vijana akaamua kumuingiza katika timu ya wakubwa na kumfanya kuwa chaguo la tatu.

Katika kipindi cha majira ya joto mwaka huo, klabu nyingine ya England, Wigan ilimnyemelea kwa uhamisho wa kudumu lakini Atletico walikataa ofa yao. Wakati kipa wa kwanza wa Atletico, Sergio Asenjo alipoenda katika majukumu ya timu yake ya taifa, De Gea aliitwa kuwa msaidizi wa kipa wa pili, Roberto.

Aliichezea Atletico mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 mnamo Septemba 30, 2009 akiingia uwanjani dakika ya 27 baada ya Roberto kuumia katika pambano la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Porto ugenini. De Gea alipigwa mabao mawali katika ushindi wa mabao 2-0 wa Porto.

Kuumia kwa Roberto kulimaanisha kuwa De Gea alipewa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza ya La Liga. Baada ya kipa Asenjo kurudi na kuanza kufanya makosa, huku kocha mpya Quique Flores akiwasili, De Gea alianza kuwa kipa wa kudumu msimu wa 2009–10.

Kuanzia hapo aliisaidia Atletico kutwaa taji la Europa pamoja na Super Cup.

Ferguson amfungia kazi, amnasa

Katika nusu ya kwanza ya mwaka 2011 kulikuwa na uvumi mwingi kuhusu ni kipa gani angeziba nafasi ya kipa aliyestaafu wa Manchester United, Edwin van der Sar. Macho yalielekezwa zaidi kwa De Gea na baadhi ya makipa wengine.

Mei 24, 2011 katika pambano la kumuaga mlinzi Gary Neville dhidi ya Juventus, kocha wa Manchester United wakati huo, Sir Alex Ferguson alidai kwamba dili la kumleta De Gea Old Trafford lilikuwa limekamilika.

Hata hivyo wawakilishi wa De Gea walikanusha kauli ya Ferguson huku pia menejimenti ya Atletico ikikanusha. Hata hivyo baada ya De Gea kuiongoza Hispania kutwaa michuano ya Euro chini ya umri wa miaka 21, De Gea alionekana Manchester akipimwa afya mnamo June 27. Juni 29 United ilithibitisha kuwa ilikuwa imemnunua De Gea kwa dau la Pauni 17 milioni ambazo zilikuwa rekodi kwa kipa.

Aanza na nuksi, ageuka shujaa.

De Gea alicheza mechi yake ya kwanza katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Chicago Fire mechi ya kirafiki ya mwanzo wa msimu mnamo Julai 23, 2011. Mechi yake ya kwanza ya kimashindano ilikuwa ni katika pambano la ngao ya hisani dhidi ya Manchester City Agosti 7, 2011.

Katika pambano hilo alifungwa kizembe kwa bao la kichwa na Joleon Lescott kabla ya kufungwa bao la mbali na Edin Dzeko na kuifanya City iongoze 2-0 hadi mapumziko. Hata hivyo kipindi cha pili United iligeuza kibao na kushinda mechi hiyo kwa mabao 3–2. Wiki iliyofuata alicheza pambano lake la ligi na kukosolewa kwa kuwa dhaifu katika kuokoa shuti la Shane Long wa West Bromwich na kuruhusu bao. Hata hivyo Man United walishinda 2-1. Kuanzia hapo mpaka sasa, De Gea ameichezea United zaidi ya mechi 100 na kutwaa taji la ubingwa wa England mwaka 2013.

Mrithi wa Casillas jumla

De Gea alikuwa nahodha wa kikosi cha Hispania kilichotwaa michuano ya Euro chini ya umri wa miaka 21 mnamo mwaka 2011 na mwaka 2013. Vile vile alishiriki katika michuano ya Olimpiki.

Aliteuliwa katika kikosi cha awali cha Hispania ambacho kilishiriki michuano ya kombe la dunia nchini Afrika Kusini mwaka 2010 lakini jina lake lilikatwa baadaye. Mwaka huu alikuwepo katika kikosi cha Hispania kilichoshiriki Kombe la Dunia nchini Brazil akiwa msaidizi wa Iker Casillas.

0 comments:

Post a Comment