![]() |
| Kikosi cha Simba SC kikiwa mazoezini kujiandaa na vpl. |
Achana na kurejea kwa kikosi hicho kilichoifunga Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe, Desemba 13, kocha wake Patrick Phiri amejiamini kwa kambi hiyo na kusema kwa sasa hakuna haja ya matokeo ya sare kutokana na usajili uliofanywa.
Simba inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi tisa, ilitoka sare katika mechi sita mfululizo za ligi hiyo kabla ya kuzinduka na kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 Novemba 9.
Kikosi kizima kilikuwa kambini Zanzibar kasoro mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi ambaye imeelezwa kuwa yupo jijini Dar es Salaam akiwasubiri wenzake kwa sababu alirudi kwao baada ya mechi na Yanga, ambako alikwenda kufunga ndoa na Nakalega Florence.
Waganda wengine; beki Juuko Murshid na winga Simon Sserunkuma wao walijiunga na kambi hiyo juzi Jumanne na kuanza mazoezi siku hiyo jioni na jana Jumatano asubuhi Phiri aliwapa mazoezi ya peke yao huku wenzao wakipumzishwa kwa ajili ya mechi iliyochezwa usiku wa jana kwenye Uwanja wa Amaan dhidi ya Taifa Jang’ombe inayoshika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Phiri alisema kuwa anaamini timu yake itafanya vizuri lakini atalazimika kumpa ruhusa Okwi ili arudi kwao kuendelea na fungate kisha arejee tena nchini baada ya michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayofanyika mwezi ujao.
“Hii kambi imetusaidia sana naona wachezaji wangu wameimarika zaidi, hata mazoezi ya gym yamewajenga sana, naifahamu Kagera kwamba ni timu nzuri na siwezi kuidharau lakini tuna lengo la kushinda mechi hiyo,” aliasema.
“Hatuna haja ya kutoka sare, kuthibitisha hili nadhani tutakapoingia uwanjani tutaonekana jinsi tulivyojiandaa. Timu zote tutakazokutana nazo kuanzia sasa zitaweza kuiona Simba tofuti, si ile ya awali.
“Wachezaji wote wamefika ingawa nilikuwa na wasiwasi na hawa wachezaji wapya, Okwi yupo Dar es Salaam lakini nitampa ruhusa maalumu baada ya mechi hiyo, ndoa yake ni changa hivyo nataka arudi kwao ili akija iwe moja kwa moja.”
Mzambia huyo aliongeza kusema baada ya mechi yao ya jana usiku ndipo atajua kikosi chake cha kwanza kitakuwaje baada ya usajili mpya kufanywa kwenye kikosi hicho ambacho kimeongeza wachezaji wanne; beki ya kati Murshid, winga Simon, straika Dan Sserunkuma na beki wa kulia Hassan Kessy. Katika mazoezi ya juzi usiku yaliyofanyika Uwanja wa Amaan, Phiri aliwafundisha zaidi mazoezi ya kupiga mashuti kulenga goli, kupiga krosi pamoja na penati.
Kipa Manyika Peter jana jioni alianza mazoezi mepesi baada ya kuumia shingo Jumatatu asubuhi.

0 comments:
Post a Comment