JOHN BOCCO AWANYAMAZISHA YANGA.

12/29/2014 03:04:00 pm
Sherman,Tambwe na Msuva.
YANGA iliingia uwanjani ikijua lazima ipate matokeo ya ushindi tu katika mechi dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, jana jijini Dar, lakini mpaka dakika 90 zinakamilika matokeo yakawa mabao 2-2, mashabiki wa Jangwani wakasikika wakisema: “Bahati yao”.

Mechi hiyo kali ambayo ilikuwa na msisimko kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote, ilikuwa na kasi na upinzani mkali huku Yanga ikionekana kucheza vizuri zaidi ya kipindi ilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo.

Ikiwa chini ya Kocha Hans van Pluijm, Yanga ilionyesha kandanda safi huku vijana wa Kocha Joseph Omog raia wa Cameroon nao wakionyesha kuelewana licha ya kuwa Yanga ndiyo ambao walifanya mashambulizi mengi.

Azam ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo ndiyo waliofungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Didier Kavumbagu ambaye alitumia vizuri makosa ya kipa wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ na Mbuyu Twite katika dakika ya tano.

Amissi Tambwe wa Yanga akafanya kweli kwa kusawazisha bao hilo kwa kichwa katika dakika ya saba akiunganisha vizuri krosi ya Salum Telela.Baada ya bao hilo, Yanga ambao walikuwa wakiwatumia zaidi Danny Mrwanda na Simon Msuva walionekana kuja juu kusaka bao lingine lakini ngome Azam ilikuwa imara ikiongozwa na Aggrey Morris.

Dakika ya 33 mshambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman, aliipangua ngome ya Azam na kupiga shuti hafifu lililoishia mikononi mwa kipa. Dakika ya 35 Msuva alitupia wavuni mpira lakini mwamuzi alikataa kuruhusu kuwa bao kwa madai kuwa mtoa pasi alimfanyia faulo kipa kabla ya mpira kumkuta mfungaji.

Dakika ya 43 almanusura Mrwanda aipe Yanga bao baada ya kupiga shuti kali nje ya 18 lakini liligonga mtamba wa panya na kupaa juu. Hadi mapumziko matokeo yalikuwa 1-1.Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kutawala uwanja kwa kiasi kikubwa na kufanikiwa kupata bao dakika ya 52 kupitia kwa Msuva aliyeunganisha vema krosi ya juu ya Niyonzima na kumuacha Mwadini, akiusindikiza mpira nyavuni kwa macho.

John Bocco, Azam FC.
John Bocco ambaye aliyeingia dakika ya 64 akichukua nafasi ya Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ alipeleka maangamizi kwa Yanga, ikiwa ni mechi yake ya kwanza kwenye ligi akiuunganisha vema krosi iliyochongwa na Himid Mao ambapo aliukwamisha mpira kwa kichwa na kumuacha Dida akiruka bila mafanikio.

Baada ya mchezo, Kocha wa Yanga, Pluijm alisema: “Tulistahili kushinda hususan kipindi cha kwanza, tulimiliki mchezo kwa kiwango kikubwa, lakini tulifanya makosa madogomdogo hata hivyo mechi ilikuwa ngumu, lakini tunajipanga na mechi ijayo.”

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Joseph Omog alisema: “Mechi ilikuwa nzuri na tulitaka ushindi wa lazima lakini bahati haikuwa yetu ila yote kwa yote tunajipanga na mechi ijayo.”

KADI
Wachezaji waliopata kadi za njano ni Tambwe na Oscar (Yanga SC), Erasto Nyoni (Azam FC).

VIKOSI:
YANGA SC: Dida, Juma Abdul, Edward Charles/Oscar Joshua, Twite, Kelvin Yondani, Telela, Simon Msuva, Niyonzima, Tambwe/Mrisho Ngassa, Sherman na Mrwanda/Hussein Javu.

AZAM FC: Mwadini Ali, Himid Mao, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Mudathir Yahaya, Sure Boy, Kavumbagu, Kipre Tchetche/Amri Kiemba na Brian Majwega.

0 comments:

Post a Comment