MAGULU, DAN SSERUNKUMA WASHANGAZA GYM:

12/21/2014 10:49:00 pm
Sserunkuma kwenye mazoezi Gym.


Elius Maguli.


STAMINA! Mastraika wawili wa Simba wenye nguvu za miguu, Dan Sserunkuma na Elias Maguli, wamewaacha midomo wazi wasimamizi wa mazoezi ya ‘gym’ ya timu hiyo yanayoendelea pale Chang’ombe, kutokana na kuelewa programu zote zinazotolewa, tofauti na wachezaji wengine ambao mpaka wasimamiwe.

Mkurugenzi wa gym hiyo, Payas Moremi ambaye pia ndiye amekuwa akisimamia mazoezi ya Simba, amesema Maguli na Dan wamekuwa ‘wakimuendea’ mbele kwa kila zoezi analolitoa, hali inayoonyesha kuwa tayari wanajua.

Mbali na uelewa wao, pia amewataja Awadh Juma na Nassor Masoud ‘Chollo’ kuwa ndiyo wamekuwa na ‘passion’ ya mazoezini ambapo wanajituma zaidi katika lile kundi la kusubiri kusimamiwa.
Aidha, katika hali ya kushangaza, kwenye mazoezi ya jana, Dan aliwaacha hoi watu baada ya kunyanyua nondo ya uzito wa kilo 75 kwa kushuka nayo mara 15.

“Daah..! huyu jamaa hatari, kubeba kilo 75 na kushuka nayo mara 15 kwa mchezaji siyo kitu rahisi kama unavyoitamka, ujue hapa amemaliza mazoezi mengine,” alisema Payas.

Wakati huohuo, Simba na Mwadui zinacheza mchezo wa kirafiki leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, ikiwa ni maandalizi ya Ligi Kuu Bara kwa Simba na Ligi Daraja la Kwanza kwa Mwadui ambapo Julio ametamka kuwa ataingia uwanjani bila ya kuionea huruma Simba ambayo aliwahi kuifundisha hapo awali.

Julio alisema kuwa mchezo huo anaamini utakuwa mgumu kutokana na timu zote kuwa na vikosi imara lakini akatoa angalizo kwa wapinzani wao kuwa makini kwani hawatawaonea huruma.

0 comments:

Post a Comment