PJUIJM APANGUA KIKOSI CHA MAXIMO.

12/22/2014 12:00:00 pm

KOCHA mpya wa Yanga, Mdachi, Hans van Der Pluijm, amekataa kuiangalia Yanga ya Mbrazili Marcio Maximo huku akisisitiza kuwa hataki kuangalia nyuma alipomalizia Mbrazili Marcio Maximo, badala yake ataanza kuijenga kwa njia anayoamini kuwa ni sahihi zaidi.

Pluijm amekiri kwamba, kikosi ambacho kilikuwa chini ya Maximo, kinatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kiweze kuwa bora, akasisitiza anataka kutengeneza timu bora itakayokuwa na ushindani wa kutosha kwenye ligi na hata michuano ua kimataifa.

Kocha huyo hakusita kujigamba kwamba yeye ni kocha bora na anajua anachokifanya na kwamba shauku yake ni kuona Yanga inapata mafanikio.“Najiamini kuwa mimi ni kocha bora, hivyo siogopi ushindani uliopo hivi sasa katika michuano ya ligi kuu ila kubwa zaidi nitahakikisha tunapambana kwa ajili ya kuwa na kikosi bora na cha ushindi muda wote,” alisema Pluijm.

Pluijm amekabidhiwa mikoba hiyo wiki iliyopita baada ya kusaini mkataba wa mwaka na nusu akiwa na msaidizi wake mzalendo, Charles Boniface Mkwasa.

Pluijm ambaye aliwahi kuinoa Yanga kwa miezi sita kipindi cha nyuma akitokea Berekum Chelsea ya Ghana kabla ya kutimkia Al Shoala ya Saudi Arabia ambapo alifanya kazi kwa muda mfupi na kuachana na Waarabu hao, alizungumza hayo baada ya kuulizwa kuwa anaionaje Yanga aliyokuwa nayo awali na ya sasa.

Mdachi huyo aliliambia Championi Juimatatu kuwa hataangalia nyuma kwamba Yanga ya Maximo ilikuwaje kwa kuwa si njia anayotaka kuipeleka timu hiyo.

“Unajua kwa sasa ni mapema kusema chochote kwa kuwa bado nahitaji muda kidogo kuiangalia timu na kujiandaa nayo lakini kingine siwezi kusema lolote kuhusiana na hilo kutokana na hali yenyewe ilivyo kwa sasa katika timu, nadhani unanielewa nikikwambia hivyo.

“Lakini pia nitakapoanza kuizungumzia Yanga, utaanza kulaumu katika mchezo uliopita, ila sitaangalia nyuma kuwa timu ilikuwaje na ilitengenezwa vipi kwa kuwa si sehemu ninayotaka kwenda na timu, kunaweza kuwa na mipango mipya.

“Kuna vitu vichache vya kuvifanyia marekebisho kwenye kikosi ambavyo sitakuambia kwa sasa kwa kuwa nasisitiza bado ni mapema ila nataka kuwa na kikosi chenye ushindani,” alisema Pluijm.

Pluijm ni kocha pekee wa Yanga ambaye ana rekodi ya kuwafunga Waarabu, kwani aliifunga Al Ahly ya Misri bao 1-0 jijini Dar kabla ya Yanga kutolewa kwa mikwaju ya penalti nchini Misri, hivyo Wanayanga wana imani kubwa na yeye.

0 comments:

Post a Comment