![]() |
| Kpah Sherman mshambuliaji wa Yanga. |
WAMEKWISHA! Hiyo inaweza kuwa kauli ya wanazi wa Yanga, baada ya kombinesheni ya Mrundi, Amissi Tambwe na Mliberia, Kpah Sean Sherman kuanza kuonyesha mavituzi huku ikionekana moto wa kuotea mbali na kumkuna kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Tambwe ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita, ametua Yanga baada ya ‘kumwagwa’ na Simba, huku Mliberia akijipiga kitanzi cha miaka miwili kukipiga Yanga akitokea timu ya Centikaya inayoshiriki Ligi Kuu ya Cyprus.
Katika programu ya mazoezi ya Yanga yaliyofanyika juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar, wawili hao walionekana kuelewana vizuri baada ya kupangwa timu moja, huku ‘wakigongeana’ vizuri na kuwa kivutio kwa mashabiki waliojitokeza.
Muda mwingi Pluijm alikuwa akiwasisitiza mastaa hao kutoka mataifa tofauti kucheza kwa pasi za uhakika hasa wanapokaribia langoni alipokuwa kipa mahiri wa timu hiyo, Deogratius Munishi ‘Dida’.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm alisema ‘kombinesheni’ yao ni nzuri na wanaonekana kuzoeana haraka, lakini ni mapema mno ‘kuwajaji’, alisisitiza Wanayanga wasubiri kama wiki mbili ili kupata uhakika kama kombinesheni yao itakuwa moto au watapoteana.
“Ni Kweli wanacheza kwa kuelewana, muunganiko wao ni mzuri unatia moyo, lakini ni mapema kuanza kulihakikisha hili. Ni vyema kuangalia kama programu za wiki mbili zaidi, hapo ndipo tunaweza kuthibitisha kwa asilimia mia kwamba kweli wanaelewana.
“Wanatakiwa kuelewana ‘movement’ zao, yaani mmoja akiwa eneo hili, mwingine anatakiwa kuwa wapi. Wakizoeana vizuri na kushirikiana itakuwa kombinesheni nzuri. Mambo yote hayo yanahitaji muda, ndiyo maana ninasema tuwape muda kidogo kulibaini hilo,” alisema Pluijim ambaye ni mwanachama wa Yanga.
Alipoulizwa straika wa timu hiyo, Tambwe kuhusiana na kuelewana na Mliberia huyo alisema ni mapema kulizungumzia hilo, ingawa alikiri kuwa mwanzo umekuwa mzuri kutokana na kufanya vizuri wanapokuwa timu moja katika mazoezi.
“Nashangaa tumeanza kuelewana vizuri mwanzoni kabisa, lakini bado tunahitaji muda, ni vizuri mkawa na subira kidogo,” alisema Tambwe.Imeandikwa na Nassor Gallu, Omary Mdose na Ibrahim Mussa


0 comments:
Post a Comment