PHIRI AWATOLEA UVIVU OKWI NA SSERUNKUMA.

12/29/2014 03:25:00 pm
KOCHA Mkuu wa Simba Mzambia, Patrick Phiri, ametamka kuwa haridhishwi na viwango vya washambuliaji wake Waganda, Emmanuel Okwi na Danny Sserunkuma.

Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, kwenye mchezo uliopigwa katika Uwanja Taifa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Phiri alisema kuwa washambuliaji wake wanashindwa kuzitumia nafasi nyingi wanazozipata ndani ya uwanja, na hiyo inatokana na umakini mdogo.

Phiri alisema, katika mechi dhidi ya Kagera Sugar, Sserunkuma na Okwi walishindwa kuzitumia nafasi nyingi walizozipata ndani na nje ya 18 ambazo kama wangezitumia, basi mechi hiyo isingemalizika kwa matokeo hayo ya kufungwa.

“Kama unakumbuka kwenye raundi ya saba ya ligi kabla ya kusimama, timu ilikuwa na tatizo la ulinzi, lakini nashukuru viongozi walilifanyia kazi kwa kusajili beki, lakini ninaona tatizo jipya la ushambuliaji linaanza kutokea.

“Ukiangalia mechi dhidi ya Kagera Sugar, washambuliaji walishindwa kuzitumia nafasi nyingi walizokuwa wanazipata ndani ya uwanja ambazo ninaamini kama wangezitumia vyema basi mechi isingemalizika kwa matokeo ya kufungwa.

“Ninaipongeza safu ya kiungo ambayo yenyewe ilifanya kazi vyema kuwachezesha washambuliaji kwa kuwapa pasi za kufunga na kushindwa wenyewe kuzitumia,”alisema Phiri.

0 comments:

Post a Comment